Mawakili wa Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, wamesema wameanza mchakato wa kukata rufaa kupinga hukumu ya kifungo cha miaka minne jela aliyohukumiwa kwa kosa la uchochezi, licha ya awali kushtakiwa kwa kosa la uhaini.
Mmoja wa mawakili wanaomtetea Lissu, Paul Kisabo, amesema tayari wamewasilisha taarifa ya nia ya kukata rufaa, hatua ya awali kabla ya kuwasilisha rasmi rufaa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.
Akizungumza Jumapili, Novemba 8, 2026, alipofika nyumbani kwa familia ya Lissu kwa ajili ya msiba wa baba yake, Kisabo amesema sasa wanasubiri kupatiwa nakala ya hukumu na mwenendo wa shauri ili waweze kuandaa sababu za kukata rufaa.
"Kwa sababu tuna nafasi ya kwenda mbele kwenye Mahakama ya Rufaa, sisi kama mawakili tumeshaanza mchakato wa kwenda huko kutafuta haki ya Mheshimiwa Tundu Lissu," amesema Kisabo.
Amesema taarifa ya nia ya kukata rufaa iliwasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Rugemeleza Nshala, siku ya Ijumaa, Novemba 6, ndani ya muda wa siku 10 unaotakiwa kwa hatua hiyo.
Kisabo amesema mawakili wanapinga namna Mahakama ilivyomkuta Lissu na hatia ya uchochezi, wakati shtaka lililokuwa likimkabili awali lilikuwa la uhaini.
"Mheshimiwa Lissu hakushtakiwa kwa uchochezi, hakujitetea kwa uchochezi, hakupewa taarifa kwamba wewe ulifanya uchochezi. Hakukuwa na mashitaka ya uchochezi," amesema Kisabo.
Ameongeza kuwa mawakili hao pia wanahoji uamuzi wa Mahakama kumhukumu Lissu kifungo cha miaka minne badala ya kumpa adhabu ya faini, akitaja kifungu cha 35 cha kanuni za adhabu kama sehemu ya hoja zao za kisheria.

